Hamas: Serikali mpya ya Abbas itasahilisha utekelezaji wa "Muamala wa Karne"
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekosoa uundwaji wa serikali mpya Palestina inayotawaliwa na wanachama wa chama chake cha Fath, ikisisitiza kuwa serikali ya namna hiyo itawepesisha utekeleza wa njama za Marekani dhidi ya Wapalestina zilizopewa jina "Muamala wa Karne".
Taarifa ya Hamas imesema kuwa, "Hatua hiyo ya ukiritimba ya kuunda serikali iliyozitenga harakati za Hamas na Jihadi Islami haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuwatenganisha zaidi Wapalestina."
Jana Jumamosi, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliliapisha baraza jipya lenye mawaziri 21, linaloongozwa na mpambe wake Mohammad Shtayyeh.
Taarifa ya Hamas imebainisha kwamba, lengo la Abbas ni kutekeleza mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na badala ya kuwaunganisha Wapalestina, amekuwa akifikiria kuleta mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Wapalestina.
Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Mumala wa Karne", mji wa Quds utakabidhiwa kwa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea kwao, utawala haramu wa Israel utasimamia usalama wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vivuko vya mpakani huku maeneo pekee ya Kiarabu ya Quds Mashariki yakiunganishwa na nchi ya Palestina.
Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo eneo la Ukanda wa Gaza litaunganishwa na nchi mpya ya Palestina kwa sharti la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina HAMAS kukubali kuweka chini silaha.