Maandamano ya Siku ya Wafungwa wa Kipalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5284-maandamano_ya_siku_ya_wafungwa_wa_kipalestina
Mamia ya wananchi wa Palestina jana Jumapili walifanya maandamano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza katika maadhimisho ya Siku ya Wafungwa wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2016 23:41 UTC
  • Maandamano ya Siku ya Wafungwa wa Kipalestina

Mamia ya wananchi wa Palestina jana Jumapili walifanya maandamano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza katika maadhimisho ya Siku ya Wafungwa wa Kipalestina.

Waandamanaji hao walikusanyika katika Medani ya Yassir Arafat katika mji wa Ramallah na kuelezea kughadhabishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kuwazuilia Wapalestina wakiwemo watoto wadogo katika korokoro zao chini ya mazingira ya kuogofya. Gavana wa Ramallah Laila Ghannam ambaye alikuwa miongoni mwa waandamanaji ametoa wito wa kuachiwa huru mara moja Wapalestina wanaozuiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Naye Issa Qaraqa, Waziri wa Masuala ya Wafungwa wa Palestina amemtaka Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, kwa kukanyaga haki za kimataifa na kuendelea kuwazuilia Wapalestina pasina na hatia.

Ijumaa iliyopita, Wapalestina wa maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan walifanya maandamano makubwa ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Wapalestina hao walikusanyika mbele ya jengo la Shirika la Msalaba Mwekundu katika Ukanda wa Ghaza wakitaka kuachiliwa huru Wapalestina wenzao wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa kuna karibu Wapalestina elfu saba wanaoshikiliwa mateka na utawala wa Kizayuni wa Israel katika jela za kutisha za utawala huo dhalimu.