Hamas: Mamlaka ya Ndani ya Palestina sio mwakilishi wa Wapalestina
Mahmoud al-Zahar, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina sio mwakilishi wa Wapalestina.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Hamas amesisitiza kuwa, harakati hiyo inataka kufikiwa mapatano, lakini kuna tofauti kati ya mpango wa mapatano unaoungwa mkono na makundi ya Palestina na mpango uliopo ambao una dhamira ya kuupigisha magoti Muqawama.
Al-Zahar ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Mehr la Iran na kubainisha kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina sio mali ya Wapalestina na kwamba serikali hiyo inayoongoza na Mahmoud Abbas ni ya kisaliti na isiyowakilisha maslahi ya Wapalestina walio wengi.
Jumamosi iliyopita, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliongoza hafla ya kuapishwa baraza jipya lenye mawaziri 21, linaloongozwa na mpambe wake Mohammad Shtayyeh.
Sambamba na kukosoa uundwaji wa serikali hiyo mpya ya Palestina inayotawaliwa na wanachama wa chama cha Mahmoud Abbas na kuyaweka pembeni makundi mengine ya kisiasa, afisa huyo mkuu wa Hamas ambaye ni mmoja wa waasisi wa harakati hiyo ya Muqawama amesitiza kuwa serikali ya namna hiyo itawepesisha utekeleza wa njama za Marekani dhidi ya Wapalestina zilizopewa jina la "Muamala wa Karne".
Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne", mji wa Quds utakabidhiwa kwa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea kwao, utawala haramu wa Israel utasimamia usalama wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vivuko vya mpakani huku maeneo pekee ya Kiarabu ya Quds Mashariki yakiunganishwa na nchi ya Palestina.
Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo eneo la Ukanda wa Gaza litaunganishwa na nchi mpya ya Palestina kwa sharti la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina Hamas kukubali kuweka chini silaha.