Siasa athirifu za nje, kiashiria cha serikali mpya ya Iraq
Jumamosi iliyopita Baghdad mji mkuu wa Iraq, ulikuwa mwenyeji wa kikao cha siku moja cha jumbe za mabunge ya nchi jirani zinazojumuisha Iran, Saudi Arabia, Uturuki, Syria, Jordan na Kuwait.
Adil Abdulmahdi aliarifishwa na kupitishwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Iraq katika bunge la nchi hiyo mnamo tarehe 20 Oktoba mwaka uliopita. Katika kipindi cha miezi 6 iliyopita, waziri mkuu huyo amethibitisha kwamba anazingatia sana siasa za nje kwa ajili ya kudhamini maslahi ya kiuchumi ya nchi hiyo. Rais Barham Swaleh na Muhammad al-Jalbousi Spika wa bunge la nchi hiyo pia wamethibitisha kivitendo kwamba wanaafikiana na Waziri Mkuu Abdulmahdi katika juhudi zake za kuimarisha siasa za nje kwa maslahi ya Iraq. Katika uwanja huo Barham Swaleh amefanya safari katika nchi saba za Iran, Saudi Arabia, Uturuki, Jordan, Kuwait, Imarati na Qatar katika kipindi cha siku 100 za kuapishwa kwake kuwa rais wa nchi hiyo. Muhammad al-Jalbousi naye Jumamosi iliyopita alikuwa mwenyeji wa kikao cha siku moja cha maspika wa mabunge ya Saudi Arabia, Uturuki, Syria, Jordan na Kuwait na vilevile ujumbe wa bunge la Iran. Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo Adil Abdulmahdi siku 20 zilizopita amefanya safari katika nchi za Iran na Saudi Arabia ambazo ni nchi muhimu katika eneo la Asia Magharibi. Safari na harakati hizo za kidiplomasia za kieneo za viongozi wa ngazi za juu wa Iraq zinabainisha nukta tatu muhimu.
Ya kwanza ni kwamba Iraq inataka kupunguza na hata kuondoa kabisa mizozo na mivutano na majirani zake. Akiashiria kikao cha siku moja cha mabunge ya nchi jirani mjini Baghdad, Adil Abdukmahdi Waziri Mkuu wa Iraq alisema kwamba Baghdad itafanya juhudi za kushirikiana na nchi zote jirani. Huku akisema kuwa Iraq ni kitovu kinachozikutanisha nchi zote jiran amesisitiza kwamba Baghdad itafanya juhudi zake zote kuhakikisha kwamba inashirikiana na nchi hizo zote. Nukta ya pili ni kuwa kuna mfungamano mkubwa kati ya siasa za nje na za ndani ya Iraq na kwamba siasa za nje zinafuata hali ya ndani ya nchi hiyo. Siaza za ndani zinazopewa kipaumbele na serikali ya Baghdad ni ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa na vita vilivyoanzishwa na magaidi wa Daesh. Hivi sasa Iraq inapitia kipindi cha ujenzi mpya baada ya kutokomezwa magaidi hao. Katika kipindi hiki Iraq inahitajia uwekezaji wa nje na hasa kutoka kwa majirani zake, jambo ambalo bila shaka nalo linahitajia kuwepo utulivu na kujiepusha na kila aina ya mivutano katika uhusiano na majirani hao.
Nukta ya tatu ni kwamba Iraq inajitahidi kunyanyua nafasi na hadi yake ya kieneo. Katika uwanja huo, Alaa Sakr ad-Dolfi, mbunge wa Iraq amesema kwamba kikao cha hivi karibuni cha jumbe za mabunge ya nchi jirani mjini Baghdad ni nembo ya kuanza hatua mpya ya kudhihirishwa nafasi muhimu ya Iraq katika kuleta amani na utatuzi wa migogoro ya eneo. Tofauti iliyopo kati ya mtazamo wa Iraq na nchi nyigine za Kiarabu kuhusu suala la kuimarisha nafasi yao ya kieneo ni kwamba Iraq inafuatilia suala hilo kwa njia za mani na kuboresha uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi nyingine za eneo ilihali nchi nyingine kama Saudi Arabia na Imarati zinataka kuimarisha nafasi zao za kieneo kwa kuvuruga utulivu na uthabiti wa eneo. Nchi hizo hata ziko tayari kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuendesha vita vya kichokozi na kivamizi dhidi ya nchi za eneo kwa ajili tu ya kufikia lengo hilo. Nara na kaulimbiu ya kikao cha Jumamosi mjini Baghdad pia ilisisitiza uthabiti wa Iraq na eneo zima la Asia Magharibi.