Pompeo: Safari nchini Iraq ilikuwa kuhusiana na Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameitaja safari yake ya ghafla huko Baghdad kuwa inahusiana na mivutano ya sasa kati ya nchi hiyo na Iran.
Mike Pompeo jana usiku alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdulmahdi na Rais wa nchi hiyo Barham Saleh katika ziara yake ya ghafla na ya masaa machache nchini humo. Shirika la habari la Irna limearifu kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani mwishoni mwa ziara yake hiyo mjini Baghdad alikuwa na mkutano na waandishi wa habari ambapo alidai kuwa amefanya ziara hiyo kutokana na kuongezeka harakati za Iran katika eneo.
Kwa madai ya Pompeo, wasiwasi wa Marekani kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Iraq si jambo jipya. Muhammad Ali al Hakim Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq pia ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Katika mazungumzo kati ya viongozi wa Iraq na Pompeo pande mbili zimejadili kuhusu uhusiano wa pande mbili, matukio ya karibuni kuhusu usalama wa eneo na mapambano dhidi ya ugaidi. Kabla ya safari hiyo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni huko Baghdad; vyombo vya habari vilitangaza kuwa Pompeo alikuwa amefuta safari yake nchini Ujerumani kwa ziara ambayo haikutangazwa.