Wapalestina 3 wauawa shahidi na Wazayuni kuelekea Siku ya Nakba
Kwa akali Wapalestina watatu wameuawa shahidi katika wimbi jipya la Maandamano ya Haki ya Kurejea, huku maadhimisho ya Siku ya Nakba ya kumbukumbu ya mwaka wa 71 tangu kukaliwa kwa mabavu Palestina yakijongea.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliwafyatulia risasi waandamanaji wa Kipalestina waliokuwa wakiandamana katika uzio wa Ukanda wa Gaza hapo jana baada ya Sala ya Ijumaa, ambapo watatu miongoni mwao waliuawa shahidi.
Iran Press imenukuu shirika la habari la Xinhua lililoripoti kuwa, Wapalestina wengine kadhaa wamejeruhiwa katika maandamano hayo, ambayo pia yalikuwa ya kupinga njama ya Marekani dhidi ya Wapalestina, iliyopewa jina la "Muamala wa Karne".
Hiyo jana pia, Wizara ya Afya ya Gaza iliripoti kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi na jeshi katili la Israel tokea Maandamano ya Haki ya Kurejea yalipoanza mwaka jana hadi sasa imefikia watu 304, huku wengine 17,301 wakijeruhiwa.
Maandamano ya "Haki ya Kurejea" yalianza rasmi tarehe 30 Machi mwaka jana 2018 na yamekuwa yakifanyika karibu kila Ijumaa.
Hii ni katika hali ambayo, Wapalestina 31 waliuawa shahidi na wengine 177 kujeruhiwa baada ya mapigano mapya baina ya makundi ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni kujiri kwa muda wa siku nne kuanzia Ijumaa iliyopita kufuatia hujuma ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Baada ya kughusubiwa ardhi za Palestina mnamo Mei 15 mwaka 1948, Wazayuni walianzisha operesheni ya kuwatimua hatua kwa hatua mamia ya maelefu ya Wapalestina kutoka ardhi zao za jadi, na Wapalestina wanatambua Mei 15 kama Siku ya Nakba.