Mamilioni ya Wapalestina washiriki maandamano ya "Siku ya Nakba"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53511-mamilioni_ya_wapalestina_washiriki_maandamano_ya_siku_ya_nakba
Mamilioni ya Wapalestina jana walishiriki katika maandamano ya "Siku ya Nakba" ambayo ni kumbukumbu ya siku ya kukaliwa kwa mabavu Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2019 22:05 UTC
  • Mamilioni ya Wapalestina washiriki maandamano ya

Mamilioni ya Wapalestina jana walishiriki katika maandamano ya "Siku ya Nakba" ambayo ni kumbukumbu ya siku ya kukaliwa kwa mabavu Palestina.

Jumatano ya jana tarehe 15 Mei ilisadifiana na kutimia mwaka wa 71 tangu Palestina ivamiwe na kukaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel.

Kwa mnasaba huo, jana shule, vyuo vikuu, maeneo ya umma na biashara katika miji mbalimbali ya Ukanda wa Gaza zilifungwa na wananchi kujitokeza na kushiriki katika maandamano ya siku hiyo ya Nakba.

Siku ya Nakba

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hapo jana kwa mnasaba wa "Siku ya Nakba" ilisisitiza juu ya kupinga mpango wa Marekani uliojaa njama wa "Muamala wa Karne".

Akizungumza kwa mnasaba huo, Fawzi Barhoum, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, madhali uvamizi na ukaliaji mabavu wa ardhi za Palestina ungali unashuhudiwa, basi mapambano na muqawama nao utaendelea.

Ismail Ridhwan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS akizungumza katika maandamano hayo amesema kuwa, himaya na uungaji mkono inaoupata utawala haramuu wa Israel hauwezi kusimamisha maandamano ya Wapalestina ya kudai haki zao.

Neno 'Nakba' linakumbusha mambo mawili mabaya mno katika kumbukumbu za Wapalestina na fikra za waliowengi. Mosi, ni kuundwa utawala ghasibu wa Israel mwaka 1948 na pili kufukuzwa zaidi ya Wapalestina laki nane katika ardhi yao ya asili.