Iraq yawahukumu kifo raia wa Ufaransa waliojiunga na ISIS (Daesh)
Mahakama nchini Iraq imewahukumu adhabu ya kunyongwa raia watatu wa Ufaransa, waliopatikana na hatia ya kujiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Afisa mmoja wa Idara ya Mahakama ya Iraq ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema, raia hao wa Ufaransa walihukumiwa adhabu ya kifo jana Jumapili baada ya kuthibiti kuwa walikuwa wananchama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Watatu hao ni kati ya Wafaransa 14 ambao kesi dhidi yao zilianza kusikilizwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu. Majaji wa mahakama hiyo ya Iraq wamepinga ombi la watatu hao la kutaka warejeshwe Ufaransa kwa ajili kufunguliwa mashitaka katika nchi yao hiyo ya asili.
Serikali ya Paris haijazungumza chochote kuhusiana na hukumu hiyo ya jana, ingawaje hivi karibuni Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa aliwataja raia wa Ufaransa walioujiunga na genge la kigaidi la Daesh kama 'maadui wa taifa' na kwamba wanapaswa kuhukumiwa katika nchi wanapokamatiwa.
Huko nyuma Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa ilikiri kuwa mamia ya Wafaransa wamejiunga na kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq.
Ni vyema kushiria hapa kuwa nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa awali ziliyaunga mkono na kuyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria.