Kamisheni: Israel imewakamata watoto 16,500 wa Kipalestina
Ripoti mpya imefichua kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia mbaroni watoto 16,500 tangu ilipoanza Intifadha ya Pili mwishoni mwa mwaka 2000.
Hayo yamesemwa na Abdul-Naser Farwana, mfungwa wa zamani wa Kipalestina na mtafiti wa Kamisheni ya Masuala ya Wafungwa na Wafungwa wa Zamani, katika ripoti yake ya kurasa 26.
Amesema, "Tokea mwaka 2000 hadi 2010, kesi 700 za kukamatwa watoto wa Kipalestina ziliripotiwa kila mwaka, na kwamba kesi hizo ziliongezeka hadi 1,250 katika kipindi cha miaka 8 iliyopita."
Kadhalika amefichua katika ripoti yake hiyo kuwa, utawala haramu wa Israel umewatia mbaroni watoto zaidi ya 50,000 tokea mwaka 1967, sera ambayo iliundwa kwa lengo la kuharibu maisha na mustakabali wa watoto hao wa Kipalestina.
Kuanzia mwaka 2000 wakati ilipoanza harakati ya Intifadha ya Pili, karibu watoto 2,300 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika mashambulizi ya askari wa utawala haramu wa Israel.
Utawala haramu wa Israel unaongoza kati ya tawala zinazokiuka sheria za kimataifa kwa kuwakamata watoto, kuwahukumu na kuwapa mateso ya aina kwa aina katika jela za kutisha za utawala huo.
Jinai, ukatili na mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Palestina ni kinyume na sheria za kimataifa hususan kifungu nambari 16 cha makubaliano ya kimataifa ya haki za watoto. Kifungu hicho kinapiga marufuku mienendo yoyote ya kikatili dhidi ya watoto.