Hamas: Muamala wa karne kamwe hautofanikiwa
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" kamwe hautotekelezwa na utafeli tu chini ya kivuli cha mapambano ya taifa la Palestina.
Salah al Bardoul amesisitiza kuwa, taifa la Palestina litatumia uwezo na suhula zake zote kupambana na mpango huo wa Maraekani wa "Muamala wa Karne" na kamwe hautoruhusu mpango huo uingie katika hatua ya utekelezaji.
Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ameongeza kuwa harakati hiyo ya Kiislamu itaendelea kuheshimu misingi thabiti ya kitaifa, muqawama na mshikamano wa taifa zima la Palestina na ametoa mwito wa kuandaliwa mpango maalumu wa kitaifa wa kupambana na muamala wa karne.
Khalil al Hayyah, mjumbe mwingine wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesisitiza kuwa, wananchi wote wa Palestina wanaupinga mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na kuongeza kwamba, hata kama mpango huo umepewa jina la Palestina lakini kimsingi unalenga kutoa pigo kwa eneo hili zima hivyo nchi zote za Mashariki ya Kati zina wajibu wa kuungana kukabiliana na mpango huo.
Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas watapokonwa Wapalestina na Waislamu na utakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Vile vile mpango huo unahimiza kuwa, mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina walioko katika nchi nyingine hawana haki ya kurejea Palestina na Wapalestina watapewa ruhuswa ya kumiliki vipande vidogo vidogo tu vya ardhi vitakavyobakia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Joran na Ukanda wa Ghaza.