Nukta nne muhimu za kushindwa vikao vya Makka
Katika hali ambayo siku nne zimepita tokea kufanyika vikao vya Makka lakini bado matokeo mabaya na hata yaliyo kinyume na matarajio ya waandaaji wa vikao hivyo yangali yanaendelea kuakisiwa kieneo na kimataifa.
Nukta ya kwanza ya kushindwa kufikiwa malengo yaliyotarajiwa na waandaaji wa vikao hivyo ni kuwa kushindwa huko kulionekana wazi katika maneneo na msimamo imara wa Rais Barham Salih wa Iraq katika kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League). Katika hali ambayo Mfalme Salman wa Saudia alifungua kikao hicho kwa kuielekezea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tuhuma chungu nzima zisizo na msingi na kudai kuwa Iran ndiyo inayovuruga usalama wa Asia Magharibi, Rais Barham Salih wa Iraq alimwambia mfalme huyo usoni kwamba: 'Iran ni nchi jirani na ya Kiislamu na bila shaka usalama wake ni kwa maslahi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.'
Msimamo huo madhubuti na Imara wa Rais Barham Salih uliungwa mkono na Adil Abdul Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq ambaye alieleza kuridhishwa kwake na ujumbe wa Iraq katika kikao hicho cha wakuu wa nchi za Kiarabu mjini Makka. Suala hilo linabainisha wazi uhusiano mkongwe na wa kistratijia uliopo baina ya Iran na Iraq na pia unaashiria upinzani mkali wa mojawapo ya nchi muhimu zaidi za Kiarabu dhidi ya siasa za fitina na uibuaji mifarakano za watawala wa Saudia dhidi ya Iran.
Nukta ya pili ni kwamba ilikuwa wazi tokea mwanzoni mwa vikao vyote hivyo vya Makka kwamba havingeweza kufikia malengo yaliyokuwa yakifuatiliwa na watawala wa Riyadh na hiyo ni kutokana na ukweli kwamba katika hali ambayo hotuba zote za Mfalme Salman zilielekezwa katika kuchochea uhasama kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran, lakini wazungumzaji wengine wote katika vikao hivyo hawakujishughulisha na tuhuma hizo bali walionyesha upinzani wao dhidi ya mpango wa Muamala wa Karne ambao una madhara makubwa kwa taifa la Palestina. Wakati huo huo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kutopewa uzito suala la Palestina katika taarifa ya mwisho ya vikao hivyo na badala yake kuzingatiwa mpango wa Muamala wa Karne ni dalili nyingine ya kushindwa watawala wa Saudia kufikia malengo waliyoyakusudia. Kuhusiana na suala hilo, televisheni ya al-Mayadeen imesema: Vikao vitatu vya Makka vimethibitisha kwamba, ukiondolea mbali Imarati na Baraza la Kijeshi la Sudan, hakuna nchi nyingine iliyosimama pambeni ya Mfalme Salman.
Nukta ya tatu ni kuwa kushindwa kwa vikao hivyo kulidhihiri wazi katika matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar siku ya Jumapili tarehe pili Juni. Waziri Muhammad bin Abdulrahman Aal Thani alitangaza wazi upinzani wa nchi yake dhidi ya taarifa zilizozotolewa mwishoni mwa vikao viwili vya wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na vilevile wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Alisema kuwa taarifa hizo tayari zilikuwa zimetayarishwa na kupangwa kabla ya hata kutangazwa rasmi na bila kushirikishwa nchi zote husika.
Upinzani mkali wa Qatar dhidi ya taarifa za mwisho za vikao viwili hivyo na hasira ya Adel al-Jubair, Waziri Mshauri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia ni mambo yanayoonyesha wazi kwamba si tu kuwa tofauti za nchi mbili hizo hazijapungua bali zinaendelea kuongezeka.
Nukta ya nne ni kwamba kushindwa vikao hivyo kulidhihirika wazi pia katika picha zilizosambazwa zikimuonyesha Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan akimvunjia heshima Mfalme Salman. Mkanda wa video uliosambazwa unamuonyesha Mfalme Salman akimkaribisha Imran Khan katika ukumbi wa mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambapo baada ya kumtolea maneno makali kidogo, anaonekana akimwambia mkalimani aliyekuwa amesimama pembeni yake na Mfalme, maneno fulani na kisha kuondoka hata kabla ya kutarjumiwa maneo hayo wala kupokea jibu la Salman.
Kwa maelezo hayo, inaonekana kuwa kuandaliwa vikao kama hivyo vya pande tatu mjini Makka hakujakuwa na matunda yoyote kwa Wasaudia bali hata hakujawaletea faida yoyote ya kipropaganda.