Qatar: Saudia na Imarati zinachochea ugaidi na taharuki katika eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani amesema sera za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabi zinashadidisha ugaidi na kuchochea taharuki katika eneo la Asia Magharibi na barani Afrika.
Abdulrahman al-Thani ameyasema hayo mjini London na kuongeza kuwa, serikali ya Doha haiungi mkono sera za uhasama wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Qatar ameeleza bayana kuwa, "Mpango wa nchi mbili hizo (Saudia na Imarati) wa eti kutaka kurejesha uthabiti kwa kuziunga mkono tawala za kidikteta na mabaraza ya kijeshi katika nchi za Afrika za Libya, Sudan na Misri na katika ulimwengu wa Kiarabu huenda ikawa chachu ya ghasia na machafuko zaidi."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameashiria kuhusu sera za kiuhasama za Riyadh na Abu Dhabi dhidi ya Iran na kubainisha kuwa, "Hivi sasa wanaendelea kufuata sera zile zile za miaka mitatu iliyopita ambazo zilikosa kuzaa matunda, nadhani wakati umefika wa kuziangalia upya sera hizo."
Hali kadhalika amekariri kauli yake ya hivi karibuni kuhusu mkutano wa Makka na kusema kuwa, Qatar haikuunga mkono taarifa dhidi ya Iran zilizotolewa katika vikao vya nchi za Kiarabu na Kiislamu katika mji wa Makka nchini Saudi Arabia hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani amefafanua kuwa, "Taarifa zilizotolewa katika mikutano ya Baraza la Ghuba ya Uajemi na nchi za Kiarabu mjini Makka hazikuungwa mkono na washiriki wote wa mikutano hiyo."