Umoja wa Mataifa waunga mkono kuhitimishwa ukaliwaji mabavu ardhi za Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54136-umoja_wa_mataifa_waunga_mkono_kuhitimishwa_ukaliwaji_mabavu_ardhi_za_palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono kuhitimishwa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2019 06:19 UTC
  • Umoja wa Mataifa waunga mkono kuhitimishwa ukaliwaji mabavu ardhi za Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono kuhitimishwa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kuwa njia pekee ya kurejesha amani ya kudumu huko Palestina ni kuhitimisha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina kulikoanza mwaka 1967. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa umoja huo unaendelea kutilia mkazo kuhusu jukumu la pamoja la kuasisi nchi huru ya Palestina kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, makubaliano ya huko nyuma na sheria za kimataifa. 

Ardhi za Palestina zinazoendelewa kumegwa na Israel
 

Guterres ameyasema hayo katika hali ambayo kikao cha kiuchumi kinatazamiwa kufanyika siku chache zijazo huko Manama mji mkuu wa Bahrain kwa lengo la kuunga mkono mpango uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne." Kikao cha Bahrain ambayo ni hatua ya awali katika kutekeleza mpango huo wa Muamala wa Karne kimepangwa kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi huu wa Juni huko Manama, hata hivyo aghalabu ya nchi duniani zimetangaza kuwa zinapinga kufanyika kikao hicho. Kwa mujibu wa mpango huo uliopendekezwa na Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Kipalestina wanaoishi katika nchi nyingine hawatakuwa na haki ya kurejea katika ardhi zao za asili na Palestina itamiliki sehemu ndogo tu ya ardhi itakayosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.