Mamluki wa Sudan waendelea kuwepo katika vita vya Saudi Arabia huko Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54335-mamluki_wa_sudan_waendelea_kuwepo_katika_vita_vya_saudi_arabia_huko_yemen
Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ambao ulianza baada ya wananchi kufanya maandamano ya kila siku ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na kuongezeka umaskini, ungali unaendelea licha ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Jun 25, 2019 02:28 UTC
  • Mamluki wa Sudan waendelea kuwepo katika vita vya Saudi Arabia huko Yemen

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ambao ulianza baada ya wananchi kufanya maandamano ya kila siku ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na kuongezeka umaskini, ungali unaendelea licha ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Wasudani wanataka kuundwe serikali ya kiraia na kufanyike mageuzi ya kimsingi katika siasa za ndani na nje ya nchi. Kuwepo wanajeshi wa Sudan katika muungano wa Saudi Arabia katika vita vya Yemen na uingiliaji kati wa nchi hiyo ya kifalme na muitifaki wake, Imarati katika masuala ya ndani ya Sudan pia vimezidisha malalamiko na upinzani wa watu wa Sudan dhidi ya utawala wa kijeshi uliotwaa madaraka baada ya al Bashir kuondolewa madarakani. Baada ya matukio ya kisiasa yaliyofuatia harakati ya wananchi wa Sudan ya kumtimua al Bashir, ilitazamiwa kuwa, nchi hiyo ingejiondoa katika muungano wa vita vya Saudia vinavyoendelea kuangamiza roho za raia wa Yemen. Kinyume chake, watawala wa kijeshi wa Sudan wametangaza kuwa, watabakisha jeshi la nchi hiyo huko Yemen. Naibu Mkuu wa Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan, Mohammad Hamdan Dagalo amesema nchi hiyo itaendelea kuwepo katika muungano wa Saudia huko Yemen na amekiri kwamba, Sudan ina awanajeshi elfu 30 wanaopigana huko Yemen. Dagalo amesema pesa zilizotolewa na Saudi Arabia na Imarati mkabala wa kutumwa askari wa Sudan huko Yemen kwa ajili ya kushiriki vita, ziko katika Benki Kuu ya nchi hiyo.

Vijana wa Sudan wanaendelea kupelekwa vitani huko Yemen kwa tamaa ya fedha ya viongozi wa nchi hiyo

Askari wa Sudan walitumwa Yemen kushiriki vita vya Saudi Arabia dhidi ya taifa hilo katika kipindi cha utawala wa Omar al Bashir kwa ahadi ya kupewa misaada ya kifedha. Hatua hiyo ilipingwa vikali na wanasiasa, raia na vyama vya upinzani. Vyama vya siasa na makundi ya kiraia nchini humo pia yanaendelea kupaza sauti yakitaka kurejeshwa nyumbani wanajeshi wa Sudan walioko huko Yemen. Vyama hivyo vinasema, hatua hiyo ni sawa na kufuja rasilimali watu na fedha za taifa. Vilevile wanapinga suala la kutumwa askari wa Sudan kuua Waislamu wenzao na raia wasio na hatia huko Yemen.

Wapinzani wa Sudan wanasema, baadhi ya askari waliotumwa kushirikiana na Saudia katika vita vya Yemen ni vijana wenye umri mdogo. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, askari wengi wa Sudan wanaotumwa kupigana vita huko Yemen ni watoto wadogo wanaokusanywa kutoka katika maeneo maskini kama Darfur mkabala wa kupewa pesa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imekiri kwamba, Sudan inatumia watoto katika vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Ripoti mpya ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa: Maafisa wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Sudan wameghushi nyaraka za watoto wadogo wanaotumiwa kama wapiganaji katika vita huko Yemen. 

Vijana wa Sudan wanauawa ovyo katika vita vya Yemen

Msaada wa dola bilioni tatu uliotolewa na Saudia na Imarati kwa Baraza la Kijeshi la Mpito na misaada ya silaha na ya kijeshi kwa baraza hilo sambamba na safari za vinara wake katika nchi za Saudi Arabia na Imarati vimewashawishi kuwabakisha wanajeshi wa Sudan katika muungano wa vita huko Yemen, suala ambalo limezidisha hasira za wananchi wa Sudan wanaosema, vijana wao wanaendelea kuuliwa bure kwa sababu ya hongo na fedha za mafuta za Riyadh na Abu Dhabi. 

Mtaalamu mashuhuri wa masuala ya kisiasa wa Uingereza, Robert Fisk amezungumzia suala la kutumwa mamluki wa Kisudani huko Yemen kushiriki katika vita vya Saudia chini ya uongozi wa Mohammad Hamdan Dagalo na kusema: Waandamanaji wa Sudan wanataka kujua maafisa wanaojificha nyuma ya pazia waliofanya mapatano ya kutuma vijana wa Sudan katika makucha ya mauti huko Yemen mkabala wa dola bilioni tatu za Saudia na Imarati.