Bahrain: Tunataka kuimarisha uhusiano wetu na Israel
Bahrain ambayo ilikuwa mwenyeji wa eti mkutano wa kiuchumi wa mjini Manama baada ya kuficha kwa muda mrefu uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel, hatimaye imefunguka na kusema kuwa inataka kuwa na amani na kuimarisha uhusiano wake na utawala huo haramu.
Khalid bin Ahmed Aal-Khalifah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain amesema hayo katika mahojiano na gazeti la The Times of Israel pambizoni mwa mkutano wa eti kuimarisha uchumi wa Wapalestina uliofanyika Manama.
Kikao cha siku mbili ambacho ni hatua ya awali kwa ajili ya kutekelezwa mpango wa Muamala wa Karne, kilianza siku ya Jumanne mjini Manama, Bahrain.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain amedai kuwa, "Israel ina haki kuwepo na itaendelea kuwepo bila shaka. Israel ni sehemu ya turathi za eneo hili."
Amewataka viongozi wa utawala huo bandia wasichoke kufanya mazungumzo na kulobi viongozi wa nchi za Kiarabu, huku akieleza matumaini yake ya kufanikiwa njama za Marekani, Israel na tawala vibaraka dhidi ya Wapalestina kwa jina 'Muamala wa Karne'.
Mpango huo umekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Wapalestina wenyewe na Waislamu kote duniani. Maandamano ya kupinga mpango huo yamefanyika katika nchi kadhaa duniani kama vile Morocco, Palestina na baadhi ya maeneo ya Bahrain.