Wayemen waandamana dhidi ya ubeberu wa Marekani na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54418-wayemen_waandamana_dhidi_ya_ubeberu_wa_marekani_na_saudia
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano leo Ijumaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu ukiwemo mji mkuu Sana'a, kulalamikia ubeberu wa Marekani na mashambulizi ya kikatili ya Saudi Arabia.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 28, 2019 10:26 UTC
  • Wayemen waandamana dhidi ya ubeberu wa Marekani na Saudia

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano leo Ijumaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu ukiwemo mji mkuu Sana'a, kulalamikia ubeberu wa Marekani na mashambulizi ya kikatili ya Saudi Arabia.

Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara dhidi ya uvamizi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao umekuwa ukiwashambulia wananchi wa Yemen kwa zaidi ya miaka minne na nusu sasa.

Wameukosoa vikali utawala wa Washington ambao unaendelea kuiuzia Riyadh silaha za kila namna ambazo zinatumika dhidi ya raia wa Yemen. Waandamanaji hao wameitaka Saudia iache mara moja kumwaga damu za Wayemen.

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani na washirika wao dhidi ya watu wa Yemen tokea Machi mwaka 2015 yameua makumi ya maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, mbali na kuharibu kikamilifu asilimia kubwa ya miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. 

Wayemen wanapinga kufanywa wa kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel

Kadhalika wananchi wa Yemen wameyatumia maandamano hayo kupinga mkutano wa kuzindua Muamala wa Karne uliofanyika katika mji mkuu wa Bahrain, Manama.

Hapo jana Jumuiya ya Maulama nchini Yemen pia ilisema kuwa, msimamo wa viongozi wa Kiarabu walioshiriki mkutano wa Manama, Bahrain sio msimamo wa mataifa ya Kiislamu kuihusu Palestina.

Aidha harakati ya Ansarullah ya Yemen imeutaja mkutano huo wa Manama kama uhaini dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na kusisitiza kuwa kitendo hicho ni sawa na kujidhalilisha na kujitweza mbele wa Wazayuni.