Wayahudi wa Ethiopia waandamana kulalamikia ukatili wa polisi ya Israel
Maelfu ya Wayahudi wenye asili ya Ethiopia yaani Mafalasha wamefanya maandamano huko Tel Aviv kupinga ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa polisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wayahudi hao wa Kifalasha jana usiku walikabiliana na maafisa usalama wa Israel wakati wa maandamanao hayo, ambapo walisikika wakipiga nara dhidi ya Israel na kulaani ukatili wa polisi wa utawala huo. Waandamanaji kadhaa walitiwa mbaroni huku wengi wakijeruhiwa katika vurumai hizo.
Jumamosi iliyopita, polisi wa utawala wa Kizayuni walimuua kwa kumpiga risasi kijana aliyekuwa na umri wa miaka 18 kwa jina Solomon Tekah Myahudi mwenye asili ya Ethiopia katika mji wa kaskazini wa Haifa.
Hii ni licha ya kuwa askari polisi huyo wa Kizayuni siku ya kutekeleza mauaji hayo alikuwa mapumzikoni.
Wayahudi wenye asili ya Ethiopia wanaoonekana raia wa daraja la tatu wamekuwa wakiadamana mara kwa mara kupinga ukatili wa polisi ya Kizayuni dhidi yao. Januari mwaka huu, Mafalasha hao waliandamana kulaani hatua ya polisi kumpiga risasi kijana mwingine wa miaka 24 Myahudi mwenye asili ya Ethiopia katika mji wa Bat Yam.
Wayahudi wa Kiafrika wanaoshi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu miaka kadhaa iliyopita walishuhudiwa pia wakifanya maandamano makubwa wakipinga ubaguzi wa Israel hususan katika suala la makazi na kukodi nyumba.