Abbas apinga upatanishi wa Marekani katika mgogoro wa Palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa Palestina haiwezi kukubali upatanishi wa Marekani kati yake na utawala haramu wa Israel.
Mahmoud Abbas amemtuhumu mshauri mkuu wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner kuwa ni kidhabi na muongo na kuongeza kuwa, tangu baada ya mapatano ya Oslo hadi sasa hakukuwepo upatanishi mpya wa Wamarekani katika mgogoro wa Palestina.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa mazungumzo ya Oslo yaliendelea kwa kipindi cha miezi 8 bila ya Wamarekani kuwa na habari. Ameongeza kuwa, anataka kuieleza historia kwamba wakati wa Wamarekani walipoelewa kwamba Palestina imetia saini makubaliano ya awali walitoa pendekezo kwamba lazima mapatano hayo yaandikwe kwenye karatasi ya Kimarekani.
Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, Marekani ambayo inatayarisha mazungumzo inapaswa kwanza kutambua rasmi njia ya utatuzi ya kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.