Nouri al-Maliki: Hashdu sh-Sha'abi inadhamini usalama wa Iraq
Nouri al-Maliki, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq amesema kuwa, wapiganaji wa kujitolea wa Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi, wanadhamini usalama wa nchi hiyo.
Al-Maliki ameashiria nafasi chanya ya harakati hiyo katika kusambaratisha kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na kuongeza kwamba, kujitolea na muqawama wa wapiganaji wa harakati hiyo mkabala wa makundi ya kigaidi, kunabainisha udharura wa kuwepo kwa Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq. Kadhalika waziri mkuu huyo wa zamani wa Iraq amesema kuwa, harakati hiyo ni lazima iwe chombo kati ya vyombo vya serikali na chini ya Amiri Jeshi Mkuu wa Iraq na si kuunganishwa tu ndani ya polisi au jeshi la nchi hiyo.
Adel al Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hiyo tarehe Mosi ya mwezi huu alitoa dikrii ya vipengee 10 kwa ajili ya kuiunganisha harakati hiyo na majeshi ya Iraq. Harakati hiyo iliundwa mwaka 2014, kupitia fatwa ya kiongozi mkuu wa kidini nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani, baada ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kuvamia na kuyakalia kwa mabavu maeneo na miji kadhaa ya Iraq. Kufuatia juhudi kubwa za kimapambano hatimaye ilifanikiwa kulisambaratisha kundi hilo la kigaidi, ambapo mwaka 2016 bunge la Iraq liliiweka Hashdu sh-Sha'abi chini ya usimamizi wa amiri jeshi mkuu wa nchi hiyo.