Marekani yaiwekea vikwazo harakati ya Hashd al Shaabi ya Iraq
Naibu Rais wa Marekani amesema kuwa nchi hiyo imeamua kuwawekea vikwazo makamanda wanne waandamizi wa harakati ya wananchi ya Hashd al Shaabi ya Iraq.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al Hadath, Mike Pence alisema hayo jana katika mkutano uliopewa jina la eti uhuru wa kidini na huku akirudia madai ya kila siku dhidi ya Iran ya eti kuunga mkono ugaidi amesema: Hatuwezi kukaa tu vivi hivi kuangalia "wanamgambo" wanaoungwa mkono na Iran wanazidi kueneza hofu.
Kwa miezi kadhaa sasa Marekani inafanya njama za kushadidisha mashinikizo dhidi ya harakati ya wananchi ya Hashd al Shaabi kiasi kwamba baadhi ya makundi yaliyoko chini ya harakati hiyo yamewekwa kwenye orodha ya Marekani ya eti makundi ya kigaidi.
Hii ni katika hali ambayo hiyo hiyo Marekani imelitoa genge la kigaidi la MKO katika orodha yake ya makundi ya kigaidi licha ya kwamba genge hilo lina historia chafu ya kumwaga damu za wananchi na viongozi wa Iran.
Inasemekana kuwa, Washington inafanya njama za kuilazmisha serikali ya Iraq iibane harakati hiyo ya wananchi, lakini hadi hivi sasa imeshindwa.
Harakati ya kujitolea ya wananchi ni moja ya vikosi muhimu sana vilivyosaidia ukombozi wa ardhi za Iraq kutoka katika makucha ya magaidi hasa wa Daesh (ISIS) walioanzishwa na Marekani. Kabla ya kuundwa harakati hiyo ya wananchi, magaidi wa Daesh walikuwa wanapata nguvu siku baada ya siku licha ya Marekani kudai kuwa eti inapambana na genge hilo la kigaidi.