Rais Mahmoud Abbas: Katu Wapalestina hawataukubali mpango wa 'Muamala wa Karne'
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, katu Wapalestina hawataukubali mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne'.
Kwa mara nyingine tena Rais Mahmoud Abbas amesisitiza juu ya siasa zisizobadilika za Wapalestina za kuupinga mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne pamoja na mkutano wa Manama.
Akizungumza katika mkutano wa Kamati Kuu ya Chama cha Fat'h, Mahmopud Abbas amesema bayana kwamba, Wapalestina hawawezi kuukubali mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' ambao kimsingi umejaa njama dhidi ya taifa la Palestina.
Mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" umedharau haki za mamilioni ya wakimbizi wa Palestina, unahimiza kupokonywa silaha wanamapambano wa Palestina, unataka kuundwe nchi ya Palestina isiyo na jeshi na pia unahimiza kupokonywa Wapalestina na Waislamu mji wao mtakatifu wa Quds na kupewa Wazayuni, yote hayo ni miongoni mwa sababu za kufeli mpango huo wa Marekani hata kabla ya kuanza kutekelezwa.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, mpango wa hivi sasa wa "Muamala wa Karne" hautokuwa na thamani yoyote hasa kwa kuzingatia mshikamano wa wananchi, makundi yote ya Palestina na nchi zote zinazopigania malengo matakatifu wa Palestina katika kuupinga mpango huo.
Mkutano wa kiuchumi wa Manama huko Bahrain uliokuwa hatua ya kwanza ya kutekeleza mpango wa "Muamala wa Karne" ulifanyika tarehe 25 na 26 za mwezi uliopita wa Juni na kuushindwa kufikia malengo yake.