Bunge la Ulaya lalaani kunyongwa wanaharakati wa kisiasa Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55427-bunge_la_ulaya_lalaani_kunyongwa_wanaharakati_wa_kisiasa_bahrain
Wabunge kadhaa wa Bunge la Ulaya wamelaani hatua ya utawala wa Bahrain ya kuwanyonga wanaharakati wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2019 02:21 UTC
  • Bunge la Ulaya lalaani kunyongwa wanaharakati wa kisiasa Bahrain

Wabunge kadhaa wa Bunge la Ulaya wamelaani hatua ya utawala wa Bahrain ya kuwanyonga wanaharakati wa kisiasa nchini humo.

Wawakilishi 14 wa Bunge la Ulaya wamemwandikia barua Dr. Bahia Jawad al Jishi Balozi wa Bahrain nchini Ubelgiji wakilaani kutekelezwa hukumu ya kunyongwa Ali al Arab na Ahmad al Malali wanaharakati wawili wa kisiasa wa nchi hiyo na kutoa wito wa kukomeshwa hukumu hiyo huko Bahrain.

Wabunge wa Ulaya waliosaini barua hiyo wamemtahadharisha pia Dr. Bahia Jawad al Jishi kwamba iwapo utawala wa Bahrain utaendelea kutekeleza hukumu ya kunyonga dhidi ya wanaharakati wa kisiasa watafuatilia suala hilo ndani ya Bunge la Ulaya. Wabunge hao pia wamelaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kupuuza haki za binadamu na sheria za kimataifa.   

Ali al Arab and Ahmad al Malali walinyongwa tarehe 27 Julai mwaka huu kwa madai ya kuhusika na makundi ya kigaidi. Bahrain imekuwa ikishuhudia wimbi la maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwaka 2011. Waandamanaji wanataka kufanyike mageuzi ya kisiasa nchini humo. Wanaharakati nchini humo wanasema kuwa shaksia wengi, viongozi wa makundi mbalimbali, madaktari, walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa sekta ya umma wameteswa katika jela za Bahrain. 

 Utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukikandamiza maandamano ya amani ya wananchi ukiungwa mkono na serikali za nchi za Magharibi zikiwemo Uingereza, Marekani na kupatiwa misaada ya kijeshi na Saudia na maajenti wa usalama kutoka Imarati. 

Polisi Bahrain wakikandamiza maandamano ya wananchi