Wapalestina 5 wajeruhiwa katika makabiliano na wanajeshi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55495-wapalestina_5_wajeruhiwa_katika_makabiliano_na_wanajeshi_wa_israel
Wapalestina wasiopungua watano wamejeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika makabiliano na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 20, 2019 08:54 UTC
  • Wapalestina 5 wajeruhiwa katika makabiliano na wanajeshi wa Israel

Wapalestina wasiopungua watano wamejeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika makabiliano na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa duru za Kipalestina, baada ya mamia ya walowezi wa Kizayuni kuhujumu kaburi la Nabii Yusuf AS katika eneo la Nablus, kuliibuka makabiliano baina ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na  vijana Wapalestina ambapo, vijana watano Wapalestina walijeruhiwa.

Kwingineko, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamefamia maeneo ya Al Birh na Beit Rima huko Ramallah na pia eneo la Al Doura katika mji wa Al Khalil na kuwatia mbaroni Wapalestina 23.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni pia wamebomoa kituo cha kibiashara katika eneo la Al Doura na kupora mali zilizokuwa hapo.

Wakati huo huo Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Wakfu wa Kiislamu Palestina imetangaza kuwa walowezi wa Kizayuni wamehujumu Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds.

Wazayuni wanajaribu kuuteka msikiti wa Al Aqsa kwa uungaji mkono wa Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mji wa Quds ni mahali ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu na ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu makuu matakatifu ya Kiislamu yenye hadhi na umuhimu maalumu mbele ya Waislamu.

Mji huo ulivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967.

Mji wa QUDS

Wakati huo huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito kwa Wapalestina wote kusimama na kuungana pamoja kwa ajili ya kuuhami msikiti wa Al Aqsa.

HAMAS imetoa taarifa kuwataka Wapalestina wajitokeze na kuhudhuria kwa wingi katika maandamano makubwa ya Haki ya Kurejea ya Ijumaa ijayo na katika harakati nyingine za wananchi.

Taarifa hiyo ya Hamas imeeleza kuwa: Ijumaa ijayo ni siku ya kuulinda msikiti wa Al Aqsa, kukabiliana na mipango na njama za Marekani na Israel na kuwaunga mkono wakazi wa Quds kwa kaulimbiu ya "Tumeitika Ewe Aqsa."