Mahmoud Abbas: Marekani haisaidii juhudi za kurejesha amani Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55702-mahmoud_abbas_marekani_haisaidii_juhudi_za_kurejesha_amani_mashariki_ya_kati
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa Marekani haisaidii juhudi za kurejesha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2019 22:14 UTC
  • Mahmoud Abbas: Marekani haisaidii juhudi za kurejesha amani Mashariki ya Kati

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa Marekani haisaidii juhudi za kurejesha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mahmoud Abbas ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mjini Berlin na kuongeza kuwa serikali ya Washington imeondoa maudhui kama ya Quds (Jerusalem), wakimbizi, mipaka, ujenzi wa vitongoji vya walowezi na usalama katika meza ya mazungumzo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, badala yake, Marekani imeweka mezani masuala ambayo yanakinzana na sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Vilevile amezitaka nchi wanachama katika Umoja wa Ulaya kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina na kuunga mkono haki ya mataifa mbalimbali ya kujiamulia masuala ya mustakbali wao na kukomesha uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina. 

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametilia mkazo udharura wa kutatuliwa hitilafu zilizopo ktika eneo la magharibi mwa Asia na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kusema: Mwaka 2018 Ujerumani ilitoa Euro milioni 110 kwa ajili ya kukarabati na koboresha hali ya Wapalestina.

Mahmoud Abbas na Angela Merkel

Baada ya Donald Trump kushika madaraka ya nchi huko Marekani, kiongozi huyo alikata misaada yote ya kibinadamu kwa Wapalestina kwa lengo la kuwashinikiza na kuwalazimisha kukubaliana na ujuba na matakwa yasiyo halali ya utawala wa Kizayuni wa Israel.