Wazayuni watishia kuushambulia Ukanda wa Ghaza kabla ya uchaguzi wa bunge
Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameitishia kuwa eneo la Ghaza litashambuliwa kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge la utawala huo siku ya Jumanne.
Gilad Erdan mapema wiki hii aliashiria mapambano ya wanamuqawama wa Palestina yanayoendelea kupitia maandamano ya Haki ya Kurejea na kudai kuwa, viongozi wa Israel wamekubaliana kutekeleza oparesheni za kijeshi katika siku zijazo.
Akizungumza na televisheni ya kanali ya 13 ya Israel, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Ijumaa iliyopita alitishia kuushambulia Ukanda wa Ghaza. Netanyahu alisema kuna uwezekano oparesheni hiyo ikafanywa kabla ya uchaguzi wa bunge wa Israel.
Vitisho hivyo vya viongozi wa ngazi ya juu wa utawala wa Kizayuni vimetolewa kabla ya uchaguzi wa bunge wa utawala wa Kizayuni uliopangwa kufanyika kesho Jumanne.
Erdan na Netanyahu wote wanatoka katika chama cha Likud na kwa kuzingatia kudhoofika chama hicho, viongozi hao wa utawala ghasibu wa Israel wanajaribu kutumia kila mbinu ili kujipatia kura zaidi katika siku hizi chache zilizosalia hadi kufanyika uchaguzi huo wa bunge.