Waziri Mkuu wa Iraq: Israel ndiyo inayoishambulia Hashdu Shaabi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56351-waziri_mkuu_wa_iraq_israel_ndiyo_inayoishambulia_hashdu_shaabi
Waziri Mkuu wa Iraq ameubebesha dhima utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutekeleza wimbi la mashambulizi dhidi ya harakati ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu ya Hashdu Shaabi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 01, 2019 07:56 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq: Israel ndiyo inayoishambulia Hashdu Shaabi

Waziri Mkuu wa Iraq ameubebesha dhima utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutekeleza wimbi la mashambulizi dhidi ya harakati ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu ya Hashdu Shaabi.

Adil Abdul-Mahdi alisema hayo jana Jumatatu katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kuongeza kuwa, "Ishara zote zinazonesha kuwa hakuna mtu anayetaka vita katika eneo la Asia Magharibi isipokuwa Israel."

Amebainisha kuwa, uchunguzi wa serikali ya Iraq umebaini kuwa jeshi la utawala haramu wa Israel ndilo limefanya msururu wa mashambulizi dhidi ya Hashdu Shaabi. Amekumbusha kuwa, harakati ya Hashdu Shaabi ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Iraq alisaini dikrii ambayo kwa mujibu wake, vikosi hivyo vya kujitolea vitakuwa chini ya kamanda mkuu wa majeshi yote ya Iraq na vitafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopasishwa katika bunge la nchi hiyo. 

Wanamapambano wa Hashdu Shaabi wakiwa katika operesheni

Serikali ya Baghdad inajiandaa kuwasilisha faili la malalamiko yake dhidi ya chokochoko hizo za Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mapema mwaka huu, gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post liliandika kwamba Iraq imegeuka kuwa shabaha ya mashambulizi ya kijeshi ya Tel Aviv katika kile kinachodaiwa na utawala huo wa Kizayuni kwamba ni kuizuia Iran kuwa na mawasiliano ya ardhini na nchi mbili za Syria na Lebanon.