Harakati ya Kiislamu Iraq: Marekani ina mkono katika machafuko ya Iraq
Harakati ya Kiislamu nchini Iraq imetangaza kuwa, serikali ya Marekani inahusika na machafuko ya sasa nchini humo kutokana na kutoridhishwa kwake na siasa za serikali ya Baghdad.
Hussein al Asadi ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Iraq amesema kuwa, kwa sasa kunashuhudiwa njama kama ile iliyotekelezwa mwaka jana katika mji wa Basra. Ameongeza kuwa, Marekani hairidhishwi na siasa za serikali ya sasa ya Iraq na kwamba katika mazungumzo yake ya asimu ya hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alimtaka Waziri Mkuu wa Iraq Adil al Mahdi, afute safari yake nchini Uchina kwa ajili ya kusaini mikataba ya kiuchumi na serikali ya Beijing akisema kwamba, suala hilo yumkini likatia doa katika uhusiano wa Baghdad na Washington.
Wakati huo huo mkuu wa mkoa wa Najaf nchini Iraq ametangaza kuwa, vyombo vya usalama vimewakamata wanachama wa timu iliyokuwa imeingia katika eneo la kale la mji huo lenye makazi ya kiongozi mkuu wa kidini kwa ajili ya kuanzisha ghasia na machafuko.
Ripoti zinasema askari usalama wamefanikiwa kuzima njama hiyo na kuwatia nguvuni wahusika.
Katika upande mwingine mwakilishi wa kiongozi mkuu wa kidini wa Iraq na hatibu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Karbala, Sayyid Ahmad al Swafi ameashiria ghasia za hivi karibuni nchini Iraq na kusema serikali inapaswa kutekeleza vyema majukumu yake yote kuhusiana na raia.
Katika siku za hivi karibuni mikoa kadhaa ya Iraq ukiwemo wa Bahgdad, imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi katika idara za serikali.
Pamoja na hayo ushahidi unaonyesho kuwa maandaano hayo ya hivi karibuni nchini Iraq hayakuibuliwa na wananchi wenyewe bali yalichochewa na maadui. Imedokezwa kuwa asilimi 79 ya jumbe zote za Twitter ambazo zimesambazwa kuhusu maandamano ya Iraq zilienezwa na watumizi wa Twitter walioko Saudi Arabia.