Rais wa Lebanon: Nitajitahidi kufanya kila niwezalo kupunguza maumivu ya wananchi
(last modified Sat, 19 Oct 2019 07:43:30 GMT )
Oct 19, 2019 07:43 UTC
  • Rais wa Lebanon: Nitajitahidi kufanya kila niwezalo kupunguza maumivu ya wananchi

Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema, atajitahidi kufanya kila lililo kwenye uwezo wake ili kupunguza maumivu waliyonayo wananchi.

Rais wa Lebanon aliyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika mkutano na kundi moja la wananchi wanaolalamikia utendaji dhaifu wa serikali ya waziri mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri.

Michel Aoun amesema, amefanya kila jitihada kwa ajili ya kufanikisha kivitendo mageuzi ya lazima yanayohitajika nchini Lebanon, kupambana na ufisadi na kutatua matatizo mengine, na akaongeza kwamba, serikali itachukua hatua kadhaa kuhusiana na yale yanayolalamikiwa na wananchi.

Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri amesema, nchi hiyo inapita katika kipindi kigumu ambacho hakijawahi kushuhudiwa na kusisitiza kwamba serikali itajitahidi kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.

Maandamano ya kupinga serikali katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut

Hariri ameeleza kuwa, serikali yake inakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na madeni, gharama za umeme, gharama za ulipaji mishahara pamoja na kutoweka uwekezaji na vitega uchumi nchini humo.

Waziri Mkuu wa Lebanon aidha ametoa muhula wa masaa 72 kwa wadau wa serikali ya umoja ya nchi hiyo kuhakikisha wanachukua hatua za kutatua hali mbaya ya mgogoro uliopo.

Miji mbali mbali ya Lebanon na hasa mji mkuu Beirut tangu Alkhamisi jioni imekuwa ikishuhduia maandamano ya kupinga serikali, ya wananchi wanaolalamikia utendaji dhaifu wa serikali ya Hariri kuhusiana na hali ya maisha na uchumi pamoja na kodi mpya zilizotangazwa na serikali hiyo.

Wiki mbili zilizopita pia Beirut na miji mingine kadhaa ya Lebanon ilikuwa uwanja wa maandamano ya kupinga serikali.../

Tags