Oct 29, 2019 02:54 UTC
  • Wanajeshi wa Marekani warejea kaskazini mashariki mwa Syria

Mamia ya wanajeshi wa Marekani ambao hivi karibuni waliondoka kaskaizni mwa Syria na kuelekea Iraq wamerejea katika kambi zao za awali huku wakiwa na zana chungu nzima.

Shirika la habari la Fars limekinukuu kituo cha Haki za Binadamu cha Syria na kuripoti kuwa wanajeshi wa Marekani zaidi ya 500 huku wakiwa na zana za kijeshi na za kilojistiki siku tatu zilizopita walirejea katika kambi yao inayopatikana baina ya Tall Tamr na Tell Beydar inayounganisha ardhi ya Iraq na barabara ya Qamishli mkoani Halab. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uwanja wa ndege wa Sarrin huko kaskazini mwa Syria pia tangu siku sita zilizopita umeshuhudia ndege kadhaa za Marekani zikiruka na kutua katika eneo hilo huku shehena mbalimbali zikipakuliwa kutoka kwenye ndege hizo ikiwa ni pamoja na zana za kijeshi na kilojistiki. 

Mwanajeshi wa Marekani akiwa kwenye gari la deraya katika mji wa Qamishli
 

Kituo hicho cha Haki za Binadamu cha Syria kiliwahi pia kuripoti kuwa, kinyume na yale yanayoripotiwa kwamba wanajeshi wa Marekani wameondoka kaskazini mwa Syria; msafara mmoja wa wanajeshi wa nchi hiyo umewasili Syria ukitokea kaskazini mwa Iraq na kuelekea mkoani Deir Zor. 

  

Tags