Ansarullah: Chaguo la kijeshi haliwezi kuleta amani Yemen na katika eneo
Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameonya kuhusu uvamizi na mashambulizi yanayofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa, chaguo la kijeshi katu haliwezi kurejesha amani nchini Yemen na katika eneo.
Abdul-Malik al-Houthi amesema hayo mjini Sana'a katika mazungumzo yake na Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na kuongeza kuwa, msimamo wa Saudia wa kushupalia uvamizi wa kijeshi umeshindwa kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo ya Kiarabu na katika eneo la Asia Magharibi.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ansarullah, Mohammed Abdul-Salam baada ya mazungumzo hayo ya jana kati ya Al-Houthi na Griffiths imesema kuwa, wavamizi hao wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.
Katika siku za karibuni, ndege za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia zimeyashambulia mara kadhaa maeneo ya makazi ya raia katika mikoa ya Sa'dah na Hajjah.
Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati (UAE) na nchi zingine kadhaa, mnamo mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, angani na baharini.
Ndege za kivita za Saudia na waitifaki wake, hadi sasa zimeshaua zaidi ya Wayemeni 16,000 mbali na kuwajeruhi makumi ya maelfu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya raia wengine wa nchi hiyo, mbali na kusababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa nchi hiyo masikini ya Kiarabu.