Hamas: Silaha za muqawama ndizo pekee zinazoitia hofu Israel
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, silaha za muqawama ndizo pekee zinazodhamini usalama wa taifa la Palestina na kuilazimisha Israel ibaki kwenye makubaliano ya kusimamisha vita.
Msemaji wa HAMAS, Khaled al Azbat alisema hayo jana katika mahojiano na mtandao wa Intaneti wa al Ahd wa Lebanon na kusisitiza kuwa, muqawama unafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea huko Palestina. Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unapaswa kuheshimu masharti ya kutoshambulia raia, kusimamisha kikamilifu uvamizi wake na kuanza hatua za kuvunja mzingiro wa Ghaza.
Ameongeza kuwa, wanajeshi wa Israel wako kwenye shabaha ya silaha za muqawama na kusisitiza kuwa, moja ya vipaumbele vikuu vya muqawama ni kulinda usalama wa raia na kama utawala wa Kizayuni utavuka mstari huo mwekundu, basi wavamizi hao wa Quds ndio watakaobeba lawama za madhara yote ya jinai zao.
Kuhusiana na jinai za Israel za kushambulia raia wa Palestina, msemaji huyo wa HAMAS amesema, jambo hilo linaonesha kufeli wavamizi hao katika taarifa zao za kijasusi na hawajui ni wapi hasa yalipo maeneo ya kiistratijia ya muqawama wa Palestina. Vile vile amesema, utawala pandikizi wa Kizayuni unafanya njama za kuhalalisha jinai zake kwa kudai kuwa, kumwaga damu za watoto wadogo, wanawake na vizee wa Palestina eti ni ushindi.
Wapalestina 34 waliuawa shahidi wakiwemo watoto wadogo watatu na mwanamke mmoja na zaidi ya wengine 110 kujeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya jeshi la Israel dhidi ya maeneo ya raia huko Ghaza. Wapalestina sita waliouawa shahidi walikuwa ni wanafunzi wa shule za msingi baada ya wanajeshi katili wa Israel kushambulia skuli 15 zikiwemo skuli mbili za Umoja wa Mataifa.