Mpalestina mwenye saratani afia jela Israel kwa kunyimwa matibabu
Raia wa Palestina aliyekuwa anaugua ugonjwa wa saratani amepoteza maisha mikononi mwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kunyimwa matibabu na dawa.
Kamisheni ya Masuala ya Wafungwa ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imelaani vikali hatua hiyo ya utawala haramu wa Israel ya kumtelekeza mgonjwa huo, huku ikitaja kifo hicho kama 'mauaji ya kliniki'.
Taarifa ya kamisheni hiyo imesema Sami Abu Diyak, aliyekuwa na umri wa miaka 37 kutoka mji wa Silat ad-Dhahr katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan alifariki dunia mapema jana Jumanne baada ya kupelekwa katika Hosptali ya Asaf Harofeh ya Israel, baada ya kupuuzwa na kutelekezwa na askari gereza wa Israel kwa kipindi kirefu.
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imesema kifo cha kijana huyo wa Kipalestina aliyekuwa anaugua ugonjwa wa kansa kimetokana na 'Sera ya Idara ya Magereza ya Israel ya kuua kwa makusudi na kwa mpangilio maalumu.'
Ripoti zinasema kuwa, hadi sasa mateka 222 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika jela za Israel, ambapo 174 miongoni mwao waliaga dunia kutokana na mateso makali.
Kwa sasa karibu Wapalestina elfu sita wanashikiliwa kama mateka katika jela za utawala haramu wa Israel. 62 miongoni mwao ni wanawake na 300 ni watoto. Mateka hao wanakabiliwa na mateso ya kimwili na kiroho, unyanyasaji na udhalilishaji na miamala ya kikatili na kinyama.