HAMAS yakaribisha kuanza upya harakati za UNRWA
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekaribisha hatua ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kuongeza kwa miaka mitatu zaidi muda wa kutoa huduma kwa wakimbizi wa Palestina.
Ijumaa usiku, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi wa kura muda wa kuhudumu UNRWA hadi mwaka 2023. Katika upigaji kura, nchi 69 zimeunga mkono azimio hilo huku nchi tatu zikijizuia kupiga kura na waliopinga azimio hilo ni Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel pekee.
Katika taarifa Fawzi Barhoum, mwanachama wa ngazi za juu wa HAMAS amesisitiza kuwa, kura ya wanachama waliowengi wa Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono kuongezwa muda wa UNRWA ni jambo ambalo litachangia kuboreka hali ya kibinadamu ya mamilioni ya wakimbizi Wapalestina. Aidha amesema kuna udharura kwa UNRWA kuendelea kutoa huduma kwa wakimbizi Wapalestina hadi pale watakaporejea katika ardhi zao za jadi.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa HAMAS amesema kupitishwa azimio hilo la Umoja wa Mataifa ni ishara ya uwajibikaji wa jamii ya kimataifa kuhusu wakimbizi Wapalestina na kuvunjwa njama za Marekani na utawala wa Kizayuni za kueneza hadaa kuhusu Wapalestina.
Fawzi Barhoum ameongeza kuwa, sambamba na hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa, umma mzima wa Kiislamu na Kiarabu unapaswa kuwasaidia Wapalestina katika mapambano yao ya ukombozi. Ameongeza kuwa kwa msaada wa nchi za Kiislamu na Kiarabu, Wapalestina wataweza kusambaratisha njama za maadui na kupata haki zao za kisheria.
Kikao hicho cha Ijumaa cha Umoja wa Mataifa kilipasisha maazimio mengine saba ya kuunga mkono Wapalestina na miongoni mwa maazimio yaliyopitishhwa ni 'kufanyika uchunguzi kuhusu taathira ya utendaji wa Israel katika hali za Wapalestina na Waarabu wengine katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu."