Israel yatishia kuwaua kigaidi viongozi wa Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine ametishia kuwaua kigaidi viongozi wa Palestina.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Israel Katz akitoa vitisho hivyo na kusema kuwa utawala wa Kizayuni unajiweka tayari kuendesha operesheni ya kuwaua kigaidi viongozi wa Palestina ili kuzuia makombora yanayorushwa kutoka Ukanda wa Ghaza.
Jumatano usiku, maroketi mawili yaliyotoka Ukanda wa Ghaza yalipiga kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Asqalan na kumlazimisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akatishe shughuli zake na kukimbilia mafichoni.
Alkhamisi asubuhi ndege za utawala wa Kizayuni zilifanya mashambulizi kadhaa katika maeneo ya makazi ya watu wa kawaida huko Ghaza.
Ikumbukwe kuwa ndege za kivita, helikopta, droni na mizinga ya Israel inafanya mashambulizi ya mara kwa mara katika Ukanda wa Ghaza na kuwalazimisha wanamapambano wa Palestina kujibu jinai hizo za Wazayuni ambazo hadi hivi sasa zimeshaua shahidi na kujeruhi maelfu ya Wapalestina wasio na hatia.
Hivi karibuni pia utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia nyumba ya Baha Abu al Ata, mmoja wa makamanda wa Brigedi za Quds, tawi la kijeshi la harakati ya Jihadul Islami ya Palestina na kumuua shahidi yeye na mkewe kwa madai ya kushiriki katika mashambulizi dhidi ya Israel.