Ripoti: Israel iliwateka nyara Wapalestina 5,500 mwaka 2019
Shirika moja la kutetea haki za wafungwa limefichua kuwa, kwa akali Wapalestina 5,500 walitekwa nyara au kutiwa mbaroni na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka uliomalizika wa 2019.
Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina (PPS) imesema, watoto wadogo 889 na mabinti 128 ni miongoni mwa wa maelfu ya Wapalestina wanaoshikilia katika vituo, korokoro na jela za utawala huo haramu.
Jumuiya hiyo imesema mateka hao wa Kipalestina ambao aghalabu yao walikamatwa katika eneo la Ukingo wa Maghairi wa Mto Jordan wanakabiliana na mateso ya kimwili na kiroho, unyanyasaji na mienendo ya kikatili na kinyama.
Taarifa ya Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina imeeleza kuwa, mateka 700 wa Kipalestina wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali, wakiwemo kumi wanaogua saratani.
Shirika hilo limesema baadhi ya wanawake ambao ni miongoni mwa maelfu ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala wa Kizayuni wa Israel wamekuwa wakifanyiwa dhulma za kijinsia na hata kubakwa.
Oktoba mwaka uliomalizika wa 2019, kundi la kutetea haki za binadamu la Palestina la Klabu ya Wafungwa wa Palestina (PPC) liliripoti kuwa, makumi ya mateka na wafungwa wa Kipalestina wameuawa kwa mateso na ukatili wa aina mbalimbali wakihojiwa na kusailiwa na maafisa wa magereza na jela za utawala haramu wa Israel.