Haitham bin Tariq Aal Said, ateuliwa kuwa Sultan mpya wa Oman
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58440
Bw. Haitham bin Tariq Aal Said ameteuliwa kuwa Sultan mpya wa Oman baada ya kutangazwa habari ya kufariki dunia Sultan Qaboos wa nchi hiyo usiku wa kuamkia leo Jumamosi.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jan 11, 2020 08:06 UTC
  • Haitham bin Tariq Aal Said, ateuliwa kuwa Sultan mpya wa Oman

Bw. Haitham bin Tariq Aal Said ameteuliwa kuwa Sultan mpya wa Oman baada ya kutangazwa habari ya kufariki dunia Sultan Qaboos wa nchi hiyo usiku wa kuamkia leo Jumamosi.

Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Haitham bin Tariq alikuwa Waziri wa Mirathi na Utamaduni wa Oman kama ambavyo ni binamu wa Sultan Qaboos. Mara nyingi alikuwa akiteuliwa na Sultan Qaboos kuwa mjumbe wake maalumu katika shughuli muhimu na aliwahi kufanya kazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Baraza Kuu la Ulinzi la Oman, mapema leo asubuhi limeitisha kikao cha dharura na ndani ya kikao hicho Haitham bin Tariq amekula kiapo rasmi cha kuwa Sultan mpya wa Oman.

Hayati Sultan Qaboos wa Oman

 

Qaboos bin Said alikuwa Sultan wa Oman kwa takriban miaka 50 na amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani akiwa na umri wa miaka 79.

Baraza Kuu la Kifalme la Oman limetangaza siku tatu za maombolezo ya umma na mapumziko rasmi nchini humo kufuatia kifo cha Sultan Qaboos.

Bendera za Oman zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku 40 kumuenzi kiongozi huyo.

Qaboos aliingia madarakani tarehe 23 Julai 1970 siku ambayo wananchi wa Oman waniita kwa jina la "Siku ya Mwamko."