Marekani kuzuia pesa za mafuta za Baghdad wanajeshi wake wakitimuliwa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58473-marekani_kuzuia_pesa_za_mafuta_za_baghdad_wanajeshi_wake_wakitimuliwa_iraq
Utawala wa Washington umetishia kuzuia akaunti za benki zenye mabilioni ya dola za Iraq, iwapo serikali ya Baghdad itakeleza mpango wake wa kuwatimua nchini humo wanajeshi wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 13, 2020 00:38 UTC
  • Marekani kuzuia pesa za mafuta za Baghdad wanajeshi wake wakitimuliwa Iraq

Utawala wa Washington umetishia kuzuia akaunti za benki zenye mabilioni ya dola za Iraq, iwapo serikali ya Baghdad itakeleza mpango wake wa kuwatimua nchini humo wanajeshi wa Marekani.

Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Marekani la The Wall Street Journal ambalo limenukuu baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Baghdad wenye ufahamu kuhusu kadhia hiyo.

Maafisa hao ambao hawakutaka kutaja majina yao wameliambia gazeti hilo la Marekani kuwa, Washington imesema kuwa itafunga akaunti kuu ya serikali ya Baghdad katika Benki Kuu ya Marekani mjini New York, ambayo inahifadhi mapato ya mafuta ya Iraq kutoka nchi mbalimbali iwapo Baghdad itawafukuza wanajeshi wa US.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Donald Trump kudai wazi wazi kuwa, Washington itaiwekea vikwazo sambamba na kuzuia dola bilioni 35 za Iraq zilizoko kwenye akaunti za benki za Marekani, iwapo itawafukuza maelfu ya wanajeshi wa US walioko katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Bunge la Iraq lililoidhinisha kufukuzwa nchini humo askari vamizi wakiwemo wa US

Jumapili ya Januari 5, Bunge la Iraq lilipiga kura na kupitisha mpango uliopendekezwa na wabunge wa kuhitimisha makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na Marekani na kuwataka wanajeshi wa nchi hiyo waondoke nchini humo.

Bunge hilo lilichukua hatua hiyo baada ya jeshi la Marekani kutumia ardhi ya nchi hiyo ya Asia Magharibi kutekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na naibu mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la Hashdu Sha'abi.