Syria: Taathira za kuuawa Shahidi Qassem Soleimani zitaendelea kwa miaka mingi
Mshauri wa Kisiasa na Vyombo vya Habari wa Rais Bashar al-Assad wa Syria amesisitiza kwamba taathira za kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC, zitaendelea kwa miaka mingi.
Bouthaina Shaaban ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya Lebanon ya Al-Manar na kuongeza kwamba hatua zote za Rais Donald Trump wa Marekani zinafanyika kwa ajili ya kudhamini maslahi ya utawala haramu wa Israel. Ameongeza kwamba, kumuua kigaidi mbeba bendera ya muqawama lilikuwa takwa la utawala wa Kizayuni ambalo Trump alilitekeleza kibubusa kwa madhumuni ya kutoa pigo kwa mrengo wa muqawama. Amezidi kubainisha kuwa hata hivyo uwezo, izza, utukufu na mshikamano wa muqawama umeongeza taathira ya kuchukiwa jinai hiyo ya kigaidi ya Marekani.

Aidha Mshauri wa Kisiasa na Vyombo vya Habari wa Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa uamuzi wa bunge la Iraq wa kuwatimua askari vamizi wa Marekani kutoka ardhi ya nchi hiyo na pia jibu kali la mashambulizi ya makombora la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Marekani, ni majibu muhimu sana na kusisitiza kwamba kupunguzwa matamshi makali ya vitisho ya Trump, ni njama zake za kujaribu kupunguza ukali wa kosa lake kubwa alilolitenda. Usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 mwezi huu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye alikuwa ameelekea nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, akiwa pamoja na Naibu Mkuu wa harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi Abu Mahdi Al-Muhandis na wanamuqawama wengine wanane waliuliwa shahidi baada ya msafara wa magari yaliyowabeba kulengwa na makombora ya majeshi ya kigaidi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.