Wakimbizi wengine 1,312 wa Syria warejea nchini kwao
Kituo cha maridhiano cha Russia nchini Syria kimetangaza kuwa wakimbizi 1,312 wa Syria waliokuwa katika nchi jirani wamerejea makwao.
Taarifa iliyotolewa jana na kituo hicho imeeleza kuwa, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, wakimbizi 205 waliokuwa Lebanon na wengine 1,107 waliokuwa nchini Jordan wamewasili huko Syria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu tarehe 18 Julai 2018 hadi sasa, wakimbizi 480,000 wa Syria wamerejea nchini humo kutoka nchi kadhaa jirani.
Kufuatia mafanikio makubwa liliyopata jeshi la Syria ya kuyashinda magenge ya kigaidi na kurejesha kwa kiwango fulani amani na usalama nchini humo, wakimbizi wa Syria wanaendelea kurudi kwenye makazi yao.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makali yaliyofanywa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani pamoja na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Mamlioni ya Wasyria wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na athari za mgogoro huo.
Hata hivyo kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa Russia, jeshi la Syria limefanikiwa kusambaratisha na kuhitimisha uwepo wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) nchini humo.
Magenge mengine ya kigaidi yanaendelea kuangamizwa na kutokomezwa nchini Syria.../