Mohammed Tawfiq Allawi, ateuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58646-mohammed_tawfiq_allawi_ateuliwa_kuwa_waziri_mkuu_mpya_wa_iraq
Duru za habari nchini Iraq zimetangaza kuwa, aliyekuwa waziri wa Mawasiliano, Mohammed Tawfiq Allawi ameteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-23T08:13:53+00:00 )
Jan 21, 2020 03:50 UTC
  • Mohammed Tawfiq Allawi, ateuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq

Duru za habari nchini Iraq zimetangaza kuwa, aliyekuwa waziri wa Mawasiliano, Mohammed Tawfiq Allawi ameteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa duru hizo, baada ya wiki kadhaa za vuta nikuvute za kisiasa, Rais Barham Salih wa Iraq jana usiku alimtangaza Mohammed Tawfiq Allawi kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2003 hadi sasa, Allawi alikuwa mbunge katika duru mbili za bunge la Iraq. Aidha alikuwa waziri wa mawasiliano katika serikali ya Nouri al-Maliki.

Inasemekana kuwa waziri mkuu huyo mpya wa Iraq ameteuliwa miongoni mwa shakhsia watatu waliokuwa wamependekezwa kushika wadhifa huo.

Mohammed Tawfiq Allawi

Mohammed Tawfiq Allawi alisomea uhandisi wa usanifu majengo katika chuo kikuu cha Baghdad, lakini alilazimika kukatisha masomo baada ya kufuatiliwa kukamatwa na serikali ya dikteta Saddam Hussein. Alielekea uhamishoni nchini Lebanon ambako alikamilisha masomo yake ya shahada ya kwanza kabla ya kuondoka nchini humo na kuelekea Uingereza.

Itakumbukwa kuwa aliyekuwa waziri mkuu wa Iraq Adil Abdul-Mahdi alijiuzulu wadhifa huo Novemba 30 mwaka uliopita kufuatia maandamano ya upinzani ya wananchi yaliyofanyika katika miji kadhaa ya nchi hiyo, na tangu baada ya kujiuzulu amekuwa akiongoza serikali ya mshikizo wakati nchi hiyo inangojea kuteuliwa waziri mkuu mpya.../