Wapalestina 3 wauawa shahidi na jeshi la Israel Ukanda wa Gaza
Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi kwa kuwapiga risasi Wapalestina watatu katika uzio wa Ukanda wa Gaza.
Vyombo vya habari vya utawala huo haramu vimeripoti kuwa, Wapalestina hao waliuawa usiku wa kuamkia leo eti kwa kujaribu kuvuka mpaka na kuingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Msemaji wa jeshi la Israel anadai kuwa, Wapalestina hao waliingia Israel baada ya kuvuka mpaka wa Gaza na kuwarushia vilipuzi wanajeshi wa utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa Jumuiya ya Taifa ya Familia za Kipalestina, Wapalestina 149 waliuawa shahidi na askari wa utawala haramu wa Israel mwaka uliopita wa 2019, ambapo asilimia 74 miongoni mwao walikuwa wanatoka Ukanda wa Gaza.
Mohammed Sbeihat, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya kutetea haki za Wapalestina amesema kuwa, asilimia 23 ya Wapalestina waliouawa shahidi ni watoto wadogo.
Mauaji haya yanaendelea katika hali ambayo, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amesema kuwa umoja huo utaendelea kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya Wapalestina katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na kutafuta suluhisho la muda mrefu ikiwa ni pamoja na kukomesha mzingiro wa Gaza.