Wapalestina wakariri upinzani wao kwa "Muamala wa Karne wa Marekani"
Vyama na makundi ya Palestina yamekariri upinzani wao kwa mpango uliopendekezwa na Marekani uliopewa jina la "Muamala wa Karne" eti kwa ajili ya kutatua mzozo kati ya Wapalestina na Israel ambao Rais Donald Trump amepanga kuuzindua wiki hii.
Msemaji wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Nabil Abu Rudeineh amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina hawataruhusu kutekelezwa mpango huo wa Muamala wa Karne. Amesema uongozi wa Palestina unaoungwa mkono na wananchi, utazishinda njama zote zenye lengo la kusambaratisha malengo ya Wapalestina.
Abu Rudeinah amesema kuwa, serikali ya Palestina itaitisha mikutano kadhaa pamoja na harakati na makundi ya Kipalestina na kutangaza upinzani kamili wa kuchukuliwa mji mtukufu wa Quds. Abu Rudeinah ameutolewa mwito ulimwengu wa Kiarabu kuunga mkono msimamo wa Wapalestina na kuonya kuwa, mpango huo wa Trump utachochea mgogoro katika eneo magharibi mwa Asia.
Afisa mwingine wa Palestina ambaye hakutaja jina lake lijajwe amesema kuwa Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekataa mara kadhaa maombi ya Trump ya kuzungumza naye kwa simu.
Wakati huo huo Ismail Hania Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, mpango wa Muamala wa Karne utashindwa na kutahadharisha juu ya kuanza awamu mpya ya mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel. Amesema: "Tunatangaza kwa nguvu zote kwamba Muamala wa Karne hautaidhinishwa na njama hiyo mpya dhidi ya Palestina itagonga mwamba." Hania ametaka kuitishwe mkutano huko Cairo nchini Misri utakaoyakutanisha makundi ya Wapalestina ili kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu mpango huo uliopendekezwa na Trump.
Makundi ya mapambano ya uhuru ya Palestina yametangaza kuwa, siku Trump atakapotangaza mpango huo wa kishetani wa Muamala wa Karne itapewa jina la "Siku ya Ghadhabu ya Taifa." Vilevile yametoa wito wa kususiwa bidhaa za Marekani.
Katika upande mwingine Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) Saeb Erekat amesema kwamba Wapalestina watajiondoa katika vipengee muhimu Makubaliano ya Oslo iwapo Trump atazindua rasmi mpango wake wa Muamala wa Karne.