Saudia yaipongeza Marekani kwa mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia ameipongeza Marekani kwa kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) pamoja na wanzake kadhaa nchini Iraq.
Faisal bin Farhan Aal Saud alitoa kauli hiyo ya kifidhuli jana Jumatatu katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani na kuongeza kuwa, "naamini Marekani walichukua hatua hiyo halali kwa ajili ya kujilinda."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amebainisha kuwa, anaunga mkono matamshi ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyedai kuwa eneo la Asia Magharibi hivi sasa ni salama zaidi baada ya kuuliwa Jenerali Soleimani.
Faisal bin Farhan Aal Saud amedai kuwa, nyendo za Iran hazijabadilika baada ya hatua hiyo ya Marekani ya kumuua kigaidi Jenerali Soleimani.
Kauli ya afisa huyo wa ngazi za juu wa Saudia imetolewa katika hali ambayo, mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na jeshi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq mnamo Januari 3 yaliughadhabisha mno ulimwengu wa Kiislamu, haswa kwa kuzingatia mchango mkubwa wa Jenerali Soleimani katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo la magharibi mwa Asia hususan nchini Syria na Iraq.
Aidha matamshi hayo ya kukinzana ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia yametolewa katika hali ambayo, baada ya ukatili huo, Adel Abdul Mahdi, Kaimu Waziri Mkuu wa Iraq alisema kuwa, Luteni Jenerali Qassem Soleimani alielekea nchini Iraq akiwa mgeni rasmi wa serikali na alikwenda na ujumbe wa Saudi Arabia kuhusu mazungumzo wakati alipouawa shahidi.