Umoja wa Ulaya: Tunaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59317-umoja_wa_ulaya_tunaunga_mkono_kuundwa_nchi_huru_ya_palestina
Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, umoja huo unaunga mkono juhudi zinazofanyika kwa ajili ya kuundwa nchi huru ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2020 09:10 UTC
  • Umoja wa Ulaya: Tunaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, umoja huo unaunga mkono juhudi zinazofanyika kwa ajili ya kuundwa nchi huru ya Palestina.

Josep Borrell amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Brussels Ubelgiji na na Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambapo ameeleza kwamba, umoja huo utaendelea kuunga mkono juhudi za kuundwa nchi huru ya Palestina..

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina wamezungumzia pia hali inayowakabili hivi sasa wananchi wa Palestina hususan mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne, uchaguzi wa Palestina na anga ya kisiasa na kibinadamu inayotawala katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Mkuu huyo wa Sera za Kiigeni wa Umoja wa Ulaya alikuwa miongoni mwa shakhsia wa Ulaya walioukosoa mpango wa Marekani-Kizayuni wa Muamala wa Karne baada tu ya kuzinduliwa kwake.

Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu walizindua mpango wa Muamala wa Karne katika Ikulu ya White House. 

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.