Mahathir Muhammad apendekezwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Malaysia
Mahathir Muhammad, Waziri Mkuu wa Malaysia ambaye alijiuzulu hivi karibuni na kukabidhi barua yake kwa mfalme wa nchi hiyo, amesema atawasilisha jina lake kwa ajili ya kushika tena wadhifa huo.
Baada ya mazungumzo aliyofanya mapema leo na wajumbe wa Muungano wa Tumaini wa Pakatan Harapan (Alliance of Hope), Mahathir ametangaza kuwa, anaungwa mkono na idadi ya kutosha ya wabunge kwa ajili ya kuwania tena nafasi ya uwaziri mkuu wa Malaysia.
Na katika kile kinachoonekana kama hatua ya kuepusha machafuko na mizozano ya kisiasa ya ndani, Muungano wa Tumaini, ukiongozwa na hasimu na mpinzani wa kisiasa wa muda mrefu wa Mahathir, Anwar Ibrahim umetangaza kuwa unamuunga mkono kikamilifu mwanasiasa huyo kushika tena wadhifa wa uwaziri mkuu wa nchi hiyo.

Mahathir, mwenye umri wa miaka 94, kwa ushirikiano na Ibrahim mwenye umri wa miaka 72 walifanikisha ushindi wa Muungano wa Tumaini uliowashangaza wengi, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018, lakini misuguano ya kisiasa baina yao imeendelea kushuhudiwa na ndiyo iliyokuwa chanzo cha mgogoro wa kisiasa uliozuka nchini Malaysia hivi karibuni na kupelekea kujiuzulu Mahathir Muhammad.
Anwar Ibrahim ametangaza kuwa, anakwenda kumtaarifu mfalme wa nchi hiyo kwamba, Mahathir Muhammad ndilo chaguo pekee la Muungano wa Tumaini kwa ajili ya nafasi ya uwaziri mkuu na akawashukuru pia wajumbe wa muungano huo kwa kukubaliana na uamuzi wake huo.../