Aug 31, 2024 04:10 UTC
  • Jumamosi, 31 Agosti, 2024

Leo ni Jumamosi 26 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na 31 Agosti 2024.

Miaka 203 iliyopita katika siku kama hii, yaani tarehe 31 Agosti 1821, alizaliwa mwanafizikia na tabibu  mashuhuri Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz katika mji wa Potsdam nchini Ujerumani. Msomi huyo alihitimu masomo yake katika fani ya utabibu na mnamo mwaka 1849 alifikia daraja ya uprofesa wa fiziolojia na fizikia katika vyuo vikuu vya Berlin na Heidelberg. Japokuwa Helmholtz alitambulika zaidi kama mwanafizikia, mwanabiolojia na tabibu, lakini alikuwa mtaalamu wa hisabati na falsafa pia. Mwanafizikia huyo alitoa mchango mkubwa sana katika fani za electrodynamics na chemical thermodynamics. Katika uga wa falsafa, Herman Ludwig Ferdinand Von Helmholtz ndiye mwasisi wa falsafa ya sayansi, ambayo ni tawi la falsafa linalohusika na misingi, njia na matumizi ya sayansi. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1894 akiwa na umri wa miaka 73. ***

Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz

 

Miaka 67 iliyopita, yaani tarehe 31 Agosti 1957 nchi ya Malaysia iliyoko mashariki ya bara la Asia ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza. Watu wa Malaysia walianza kidogo kidogo kuingia katika Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa Wazungu kutoka Ulaya katika nchi hiyo ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 alipowasili nchini humo baharia wa Kireno Afonso de Albuquerque. Mnamo karne ya 17 Uholanzi iliikalia na kuitawala Malaysia; na ulipofika mwaka 1824 na kufuatia mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Uholanzi, Malaysia ikatawaliwa na Uingereza na Indonesia ikakabidhiwa Uholanzi. Uingereza iliendelea kuitawala Malaysia hadi ilipopata uhuru wake katika siku kama ya leo. ***

 

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 10 Shahrivar 1344 Hijria Shamsia, ilianzishwa kamati ya utumiaji wa nishati ya atomiki nchini Iran. Mwaka 1335, bunge la taifa la zama hizo lilipitisha mpango wa kuasisi "Kituo cha Atomiki cha Chuo Kikuu cha Tehran" na mnamo mwezi Azar 1344, mtambo wa megawati tano wa atomiki wa mafunzo na utafiti wa Iran ambao ulinunuliwa Marekani ulikuwa tayari kuanza kazi. Mwaka 1345 mtambo huo ulianza kutumika katika kituo cha utafiti cha Amir Abad Tehran na ungali unaendelea kufanya kazi hadi leo huku ukifanyiwa ukaguzi na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Mwaka 1352, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran AEOI na bila kupoteza muda likafanya mazungumzo na nchi za Ulaya kwa ajili ya uJenzi wa vinu vya nyuklia nchini. Kufuatia mazungumzo hayo, mashirika mawili ya Ujerumani na Ufaransa yalikubali kujenga mitambo miwili ya nyuklia ya megawati elfu moja katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran na kudhamini utoaji wa fueli kwa ajili ya mitambo hiyo. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kinyume na ahadi yaliyozotoa, mashirika hayo yalisitisha ujenzi wa vinu hivyo na kuondoka nchini. Hata hivyo wanasayansi vijana wa Kiirani, kwa kushirikiana na shirika la nishati ya atomiki la Russia walikamilisha ujenzi wa kiwanda cha nyuklia cha Bushehr ambacho ni cha kwanza Mashariki ya Kati kinachozalisha nishati bila kutumika kwa malengo ya kijeshi; na hadi sasa kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji wa nishati hapa nchini. ***

 

Miaka 46 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 31 Agosti 1978, Imamu Musa Sadr alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa safarini nchini Libya. Imamu Musa Sadr alizaliwa tarehe 4 Juni mwaka 1928 katika mji wa Qum nchini Iran. Baada ya kumaliza masomo, mwaka 1959 alielekea Lebanon. Wakati huo, Waislamu wa nchi hiyo walikuwa na hali mbaya sana kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kutokana na hali hiyo, Imamu Musa Sadr alichukua hatua kadhaa za msingi ili kuboresha hali zao na ndipo alipobuni taasisi ya kushughulikia masuala ya Waislamu wa Kishia iitwayo "Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon". Taasisi hiyo ilipitishwa katika bunge la nchi hiyo na yeye akachaguliwa kuwa mkuu wake. Imamu Musa Sadr alikuwa pia akiunga mkono kikamilifu mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel; na kwa ajili hiyo akaanzisha "Harakatul-Mahrumin" ambayo ililenga kutetea haki za Waislamu wa Lebanon pia. Tangu Imamu Musa Sadr alipotoweka, zimefanyika jitihada nyingi na kubwa za kupata taarifa kuhusu hatima yake, lakini hadi sasa hazijazaa matunda. ***

 

Tags