Hashdu Sha'abi yatekeleza operesheni ya mafanikio katika mikoa minne ya Iraq
Kamandi ya Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq imetangaza kumalizika kwa operesheni ya mafanikio makubwa dhidi ya magaidi katika mikoa minne ya Al-Anbar, Diyala, Kirkuk na Salahdin.
Qassem Muslih, Kamanda wa Operesheni ya harakati hiyo katika mkoa wa Al-Anbar, magharibi mwa Iraq amesema kuwa katika operesheni hiyo ambayo ilivishirikisha vikosi vinne vya 19, 18,17 na 13 vya Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi, kumeangamizwa idadi kubwa ya magaidi wa kundi la Daesh sambamba na kunasa na kudhibiti silaha zao. Naye Ali Al-Husseini, mmoja wa makamanda wa harakati hiyo pia ameelezea kujiri operesheni ya kipekee dhidi ya magaidi kwa kuyashirikisha makundi mengine ya kiusalama ya Iraq katika mikoa mitatu ya Diyala, Kirkuk na Salahdin.
Operesheni ya kuisafisha mikoa minne ya Iraq ilianza Ijumaa asubuhi. Kwa miezi kadhaa sasa mikoa ya Al-Anbar, Nainawa (Nineveh), Salahdin, kusini mwa Kirkuk na Diyala nchini Iraq, imekuwa ikishuhudia harakati za mabaki ya wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS). Harakati hizo za kigaidi zimesambaratishwa na operesheni za jeshi la serikali na wanamuqawama wa kujitolea wa Hashdu sh-Sha'abi.