Bashar Asad: Syria itaanza opesheni dhidi ya wavamizi wa Kimarekani karibuni
Rais Bashar Assad wa Syria amesema kuwa Uturuki inatekeleza maagizo ya Marekani na inafanya juu chini kuhakikisha kwamba Damascus haikomboi mkoa wa Idlib kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi.
Assad amesisitiza kuwa, jeshi la Syria hivi karibuni litaanzisha operesheni dhidi ya wavamizi wa Kimarekani mashariki mwa nchi hiyo.
Rais wa Syria amesema kuwa, hakuna uadui wa aina yoyote baina ya mataifa mawili ya Syria na Uturuki na kwamba iwapo Rais Tayyep Erdogan wa Uturuki atasitisha uungaji mkono na misaada yake kwa ugaidi, uhusiano wa nchi hizo mbili utarejea katika mkondo wake wa kawaida.
Bashar Assad amesema kuwa suala la kukombolewa eneo la Idlib linapewa kipaumbele zaidi na kuongeza kuwa, baada ya ukombozi wa eneo hilo, jehi la Syria litaelekeza nguvu zake upande wa mashariki mwa nchi na kukomboa maeneo hayo ambako raia wanachukizwa sana na uwepo wa mavamizi wa Kimarekani.
Rais wa Syria amesema Marekani na magaidi inaofadhili wamevamia na kutwaa visima muhimu vya mafuta vya nchi hiyo.
Vilevile ameashiria himaya na misaada ya Iran na Russia kwa nchi yake na kusema Damascus haitapoteza wakati kwa ajili ya kufanya mazungumzo na nchi za Ulaya kwa sababu nchi hizo zinafuata kikamilifu maagizo ya Marekani.