Hamas yalaani kuendelea kushikiliwa Wapalestina nchini Saudi Arabia
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amelaani kutiwa mbaroni viongozi wa Wapalestina na kupandishwa kizimbani huko Saudi Arabia.
Hazem Qassem alisema hayo jana usiku wakati alipohojiwa na televisheni ya al Mayadeen na kuongeza kuwa, Saudia badala ya kuwapandisha kizimbani viongozi hao wa Palestina, inapaswa kuwaachilia huru haraka kwani viongozi hao ni kigezo cha kitaifa kwa Wapaletina.
Msemaji huyo wa HAMAS ameongeza kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kulinda matukufu ya Palestina na zisimame imara kukabiliana na hatua kama hizo za Saudi Arabia.
Abdul Majid Khoudary, kaka wa Mohammed Saleh al Khoudary, mbunge wa HAMAS aliyekamatwa na viongozi wa Saudi Arabia amesema kuwa, nchi hiyo hivi karibuni ilianza kuwapandisha kizimbani watu 68 kutoka Palestina, Jordan na Saudia kwenyewe.
Kabla ya hapo pia, Sami Abu Zuhri, kiongozi mwandamizi wa HAMAS alikuwa ametangaza kuwa, hivi sasa Wapalestina 60 wanashikiliwa korokoroni nchini Saudi Arabia huku baadhi yao wakiwa ni wanachama wa HAMAS au waungaji mkono wa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu.
Kamati ya Taifa ya Kuwatetea Wapalestina Wanaotiwa Mbaroni nchini Saudi Arabia amewataka viongozi wa nchi hiyo kuwaachilia huru Wapalestina na kutowatesa na kuwashikilia kwenye seli za mtu mmoja mmoja.