Saudia yaendelea kukiuka makubaliano ya Stockholm, UN yashikwa na kigugumizi
-
Watoto wa Yemen, wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia
Saudi Arabia inaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha vita katika eneo la al Hudaydah nchini Yemen huku Umoja wa Mataiifa, badala ya kulaani kitendo hicho, umelitaka jeshi na Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah waache kusonga mbele katika mikoa ya al Jawf na Ma'rib.
Afisa mmoja wa chumba cha operesheni cha maafisa wa mawasiliano wanaofuatilia ukiukaji unaofanywa na muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia wa makubaliano ya kusitisha vita huko al Hudaydah amesema kuwa muungano huo umekiuka makubaliano ya Stockholm mara 155 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Kusimamishwa vita katika eneo la Hudaydah ni miongoni mwa vipengee vikuu vya makubaliano ya Stockholm yaliyotiwa saini Disemba mwaka 2018 chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Makubaliano hayo yaliyosainiwa na pande hasimu yalipasishwa pia katika Baraza la Usalama na baraza hilo ndilo lililochuka jukumu la kudhamini utekelezaji wake.
Saudi Arabia ilianza kukiuka makubaliano ya Stockholm masaa machache tu baada ya kutiwa saini na kuanza kutekelezwa, ilhali harakati ya Ansarullah iliheshimu makubaliano hayo na kusitisha kikamilifu mapigano katika eneo la al Hudaydah. Tangu makubaliano ya Stockholm yaanze kutekelezwa, Saudi Arabia imeyakiuka mara elfu 52 na katika kipindi hicho raia elfu 1,065 wameuawa na wengine 1567 wamejeruhiwa.
Miezi ya nyuma Saudia ilikuwa ikikiuka makubaliano ya Stockholm kwa shabaha ya kuishinikiza harakati ya Ansarullah na washirika wake. Hata hivyo iinaonekana kuwa, ukiukaji wa sasa wa Saudia na washirika wake unatokana na kushindwa kwao mtawalia katika medani za kijeshi. Operesheni kubwa ya al Bunyan al Marsus iliyoanza na mwaka huu wa 2020 na vilevile kukombolewa kwa mji wa al Hazm, makao makuu ya mkoa wa al Jawf kutoka mikononi mwa vibaraka wa Saudi Arabia ni miongoni mwa vipigo muhimu sana vya Ansarullah kwa utawala wa okoo wa Aal Saud.
Baada ya kukomboa mji wa al Hazm sasa jeshi la Yemen na wapiganaji wa Ansarullah wamekaribia sana mpaka wa Saudi Arabia na kuwa tishio kubwa zaidi kwa utawala huo wa kifalme. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, Saudi Arabia imeamua kuzidisha mashambulizi dhidi ya al Hudaydah na kukiuka makubaliano ya Stockholm ili kufidia kushindwa kwake na vipigo mtawalia vya jeshi la wapiganaji wa makundi ya kujitolea ya Yemen. Wasaudi wanadhani kwamba, ukiukaji wa makubaliano hayo utazidisha mashinikizo dhidi ya harakati ya Ansarullah na kuilazimisha isitishe kusonga mbele zaidi katika mikoa ya al Jawf na Ma'rib
Nukta nyingine ya kuzingatiwa hapa ni kuwa, Umoja wa Mataifa umeendelea kushikwa na kigugumizi na kunyamaza kimya mbele ya ukiukaji huo wa makubaliano ya kusitisha vita huko al Hudaydah. Hii ni licha ya kwamba, umoja huo unawajibika kusimamia utekelezaji kamili wa mapatano ya Stockholm.
Siku chache zilizopita Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen, Martin Griffiths ambaye alikuwa safarini mashariki mwa Yemen alitoa wito wa kusitishwa vita mara moja na bila ya masharti yoyote nchini humo. Afisa huyo wa UN alitoa wito huo baada ya mafanikio makubwa ya wapiganaji wa Ansarullah katika mikoa ya al Jawf na Ma'rib. Griffiths pia alisisitiza udharura wa kuanza mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi yote nchini humo.
Kwa sababu hiyo, Waziri wa Habari wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa nchini Yemen, Dhaifullah al Shami amekosoa nafasi ya mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa na kusema, matendo yake yanaonesha nafasi ya Uingereza katika kuigawa nchi ya Yemen.